Tuesday, July 10, 2012

Ajuza wa miaka 80, abakwa


Na SANDRA CHAO

Ajuza wa miaka themanini katika kijiji cha Madzeyani kata ya Magarini katika Kaunti ya Kilifi anauguza majeraha baada  ya kubakwa hapo jana na mwanaume wa miaka ishirini na moja.

Mkongwe huyo  alikuwa ameenda kwa shamba lake lililoko umbali wa kilomita moja unusu kutoka kwa nyumba yake mwendo wa saa tisa mchana ili kupalilia mahindi.

Kwa mujibu wa kaimu chifu wa eneo la Pumwani Bw Albert Kazungu mwanamke huyo hakuweza kupiga mayowe kwani kijana huyo aliyetambulika kama Huzuni Kahindi alimfunga mdomo na kutishia kumuua.

“Mama huyu hakuweza kupiga mayowe baada ya kutishiwa lakini aliweza kuripoti kisa hicho kwa majirani punde tu baada ya kuwasili nyumbani kwake,” alisema chifu huyo.

Bw Kazungu alisema kwamba kijana aliyemvamia mknogwe huyo alikuwa ni mchungaji kutoka kwa kijiji cha karibu cha Mpirani na alikuwa anaelekea na mifugo hao katika eneo la malishoni huko madzeyani alipokumbana na ajuza huyo na kumtendea uhalifu huo.

Ilichukuwa juhudi za wananchi na utawala wa mikoa kuweza kumkamata kijana huyo na kumpeleka katika kituo cha karibu cha polisi kilichoko Marekebuni.

“Tukishirikiana na wanakijiji tuliweza kulinda mlango wa kutokea Madzeyani na  kumkamata mshukiwa akiwaanarudi n mifugo yake na tukampeleka polisi baada ya ajuza huyo kumtambua,” alisema Bw Kazungu

Kwa sasa Kahindi anazuiliwa katika kituo cha polisi mjini Malindi huku akingojea kufunguliwa mashtaka pindi polisi wanapokamilisha uchunguzi wao.

“Kitendo hiki ni cha kwanza cha aina yake kuwahi kutokea katika eneo hili nan i matumaini yetu kwamba  afunguliwe mashtaka na kufikishwa mahakamani haraka,” chifu alieleza

Ajuza huyo alipokea matibabu kutoka kwa hosipitali kuu ya wilaya ya Malindi na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
                                 

No comments:

Post a Comment